Milipuko Iliyotokea Kampala Ni Mabomu Ya Kujitoa Muhanga- Vifo 6, Majeruhi 33 – Polisi Uganda

habari leo Milipuko Iliyotokea Kampala Ni Mabomu Ya Kujitoa Muhanga- Polisi
habari leo Milipuko Iliyotokea Kampala Ni Mabomu Ya Kujitoa Muhanga- Polisi

Jeshi la polisi nchini Uganda limeeleza kuwa milipuko miwili iliyotokea asubuhi ya leo, Novemba 16, 2021 kwenye kizuizi cha barabarani cha kuingia kwenye Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Kampala na jirani na jengo la bunge la nchi hiyo, ni mabomu ya kujitoa muhanga yaliyolipuliwa na wafuasi wa kundi la kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF).

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi, Kamishna Fred Enanga imeeleza kwamba uchunguzi wa polisi umebaini kuwa washambuliaji watatu wa kujitoa muhanga wamefariki eneo la tukio sambamba na watu wengine watatu, huku idadi ya waliojeruhiwa ikifikia 33, watano kati yao wakiwa mahututi katika Hospitali ya Mulago.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Enanga amesema kwa kupitia picha za kamera za CCTV, wamembaini mshambuliaji wa kwanza kuwa ni mwanaume aliyekuwa amebeba begi lenye milipuko ambaye alijilipua alipofika kwenye kizuizi cha kuingilia makao makuu ya polisi.

Ameongeza kuwa katika tukio hilo la kwanza lililotokea majira ya saa 10:03 (saa nne na dakika tatu) asubuhi, watu wawili walipoteza maisha papo hapo pamoja na mshambuliaji huyo wa kujitoa muhanga huku wengine 17 wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitali.

Katika tukio la pili lililotokea dakika tatu baadaye majira ya saa 10:06 (saa nne na dakika sita) asubuhi, washambuliaji wawili wa kujitoa muhanga waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki, walilipua mabomu waliyokuwa nayo mwilini nje ya Jengo la Jubilee Insurance, jirani kabisa na bunge la nchi hiyo.

Kamishna Enanga ameendelea kueleza kuwa mtuhumiwa wanne ambaye naye alikuwa akitaka kujilipua, alipigwa risasi na polisi katika eneo la Bwaise jijini Kampala kisha kukamatwa.

Habari zilizofika hivi punde ni kwamba Watu 6 wamethibitika kufariki dunia mpaka sasa huku wawili kati yao wakiwa maafisa polisi, kufuatia milipuko miwili kutokea jijini Kampala nchini Uganda karibu na Bunge na kituo cha Polisi katikati mwa jiji, leo.

Watu wengine 33 wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali za karibu kwa ajili ya matibabu na uhakiki wa waliojeruhiwa ukiendelea kufanyika ili kujua idadi.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa bomu jingine limekutwa karibu na Transifoma katika jengo la Kooki Tower na mengine mawili yamekutwa karibu na barabra ya Buganda ambapo yote yalitenguliwa huku Kitengo cha Polisi cha kupambana na ugaidi kikiendelea kutafuta mabomu mengine zaidi kama yapo ili kuyategua.

You may also like...