WIZARA YA HABARI YAVUKA MALENGO UKUSANYAJI MAPATO MWAKA 2020/2021

Innocent Bashungwa gozeep
Innocent Bashungwa gozeep

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imevuka lengo la ukusanyaji mapato  kwa kukusanya jumla ya kiasi cha Sh.1, 080,109,491 ambazo ni sawa na asilimia 113 hadi kufikia Mei, 2021 kutoka Sh. 960,000,000/= kiasi ambacho kilikadiriwa kukusanywa kwa mwaka 2020/21.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa alipowasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2021/2022.

Mafanikio ya makusanyo hayo yanatokana na usimamizi wa makusanyo ya Serikali kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya nchi na kuongezeka kwa utoaji wa huduma zinazotolewa na Wizara katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kuhusu sekta ya Habari, Waziri Bashungwa amesema “Wigo wa vyombo vya habari umeendelea kuongezwa nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya kikatiba ya kupata taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli zao”.

Hadi kufikia mwezi Mei 2021 ina idadi ya magazeti na majarida yaliyosajiliwa 257; vituo vya televisheni 43, vituo vya redio 200, televisheni mtandao 451, redio mtandao 23, blogu 122 na jukwaa mtandaoni ni 09 hatua inayoonesha namna nchi inavyoendelea kurahisisha na kuimarisha uhuru wa upatikanaji wa habari kwa wananchi.

Katika kuimarisha usikivu wa Redio za TBC,, Serikali imeendelea kuongeza usikivu wa redio kutoka Wilaya 87 mwaka 2017 hadi Wilaya 102 mwaka 2021. Miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ajili ya kuongeza mawanda na usikivu katika Wilaya za Ngara, Kyela, Ruangwa, Kilombero na Ludewa ujenzi wa mitambo ya redio ya FM unaoendelea katika Wilaya za Tanganyika, Makete, Uvinza, Mbinga na Ngorongoro itasaidia kuongezeka kwa usikivu a kufikia Wilaya 119 kati ya Wilaya zote 161 sawa na asilimia 74 ambapo matarajio ya ni usikivu wa redio kuzifikia Wilaya 134 sawa na asilimia 83 za Tanzania Bara pamoja na visiwa vya unguja na Pemba kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Katika Sekta ya Utamaduni, Wizara imeanzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ambao ulisajiliwa Septemba 30, 2020 kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa kazi za kiutamaduni na kisanaa kimitaji na kuwajengea uwezo wa kitaalamu ili kuwawezesha kuandaa bidhaa bora zinazomudu ushindani kitaifa na kimataifa.

Waziri Bashungwa amesema matumizi ya Kiswahili yanaongezeka kwa kasi duniani na  kuongeza kuwa kukubalika kwa lugha hiyo kunachagizwa na msukumo wa kustawisha lugha hiyo unaoendelea kufanywa na unaoendelea kufanywa na viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na watangulizi wao.

Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa Wizara yake iliendesha kongamano Mei 21, 2021 ambalo lilizinduliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa Tanzania katika Harakati za Ukombozi wa nchi za Afrika ili kutangaza, kuhamasisha, na kuelimisha jamii kuhusu urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika uliopo nchini.

“Mwaka 2011 Tanzania ilikabidhiwa na Umoja wa Afrika (AU) jukumu la kuratibu Programu ya Afrika ya “Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo ilipewa jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kutangaza kumbukumbu kuhusu harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo nyaraka, makaburi, majengo, mahandaki, silaha, sare, hotuba na magari kwa matumizi ya vizazi vya sasa na vijavyo ambayo makao yake makuu yapo Jijini Dar es Salaam” amesema Mhe. Bashungwa.

Katika sekta ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara imefanikiwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wasanii na wadau wa sanaa ambapo Taasisi zinazowahudumia Wasanii za BASATA, Bodi ya Filamu na COSOTA zimewekwa katika eneo moja kwenye jengo la UTUMISHI lililopo Kivukoni. Hatua hii pamoja na mambo mengine, itawapunguzia muda, kadhia na gharama wasanii wetu na wadau wengine wanaohudumiwa na Taasisi hizi.

Waziri Bashungwa amesema kuwa sekta ya Maendeleo ya Michezo nchini imeenedelea kuimarika kwa timu na wachezaji mbalimbali kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Ameendelea kusisitiza kuwa timu za mpira wa miguu nchini zinaendelea kufanya vizuri ikiwemo Timu ya Tanzanite ya Wanawake wenye umri chini ya miaka 17 imefanikiwa kutwaa Kombe la COSAFA baada ya kuzifunga timu kutoka Comoro, Afrika Kusini, Zimbwabwe na Zambia nchini Afrika Kusini mwezi Novemba, 2020 wakati mchezo wa ngumi mabondia Hassan Mwakinyo, Ibrahim Class, Salim Jengo, Tony Rashid, Bruno Tarimo na Shabani Jongo wameendelea kupeperusha vema bdndera ya Taifa.

Wakichangia hotuba hiyo, Wabunge Abbasi Tarimba, Seifu Gulamali na Nusrati Hanje wamesema sekta za Sanaa na Michezo zinakuza na kuongeza utalii nchini huku Mbunge Stanislaus Nyongo akiwasisitiza Wabunge na Watanzania kumpigia kura Msanii Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) amabye ameteuliwa kuwania tuzo ya BET ya Best International Act.

You may also like...