MAANDALIZI YA MKUTANO WA 14 WA MAWAZIRI WA EAC WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA YAANZA JIJINI ARUSHA

MAANDALIZI YA MKUTANO WA 14 WA MAWAZIRI WA EAC WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA YAANZA JIJINI ARUSHA
MAANDALIZI YA MKUTANO WA 14 WA MAWAZIRI WA EAC WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA YAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 14 Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Ngazi ya Wataalam umeanza hivi karibuni jijini Arusha ukiwashirikisha Wataalam wa Kilimo kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mkutano wa Wataalam utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 24 Juni 2021 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 25 Juni 2021.


Lengo la Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya pamoja na kupitia na kujadili masuala mbalimbali muhimu ya kisera, kikmkakati, miradi na program zinazotekelezwa katika sekta ya kilimo.
Kadhalika agenda muhimu zitajadiliwa wakati wa mkutano huo ambazo ni pamoja na Taarifa ya Usalama wa Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Mradi wa Afrika wa Kilimo cha Ushindani cha Mpunga kwa Kanda ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Mifugo; Taarifa kuhusu Mradi wa Kuzuia na Kudhibiti Sumukuvu; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Uvuvi; na Taarifa kuhusu Uhamasishaji wa Uchangiaji Rasilimali.


Awali akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Muthuki, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amezitaka Nchi Wanachama kujikita kwenye kilimo cha ushindani na kuboresha viwango vya mazao yanayozalishwa na nchi zote wanachama ili kupata soko la ndani na nje ya jumuiya la mazao hayo kwa manufaa ya wananchi wa jumuiya.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Bw. Mwabu akizungumza wakati wa mkutano huo


Pia amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuwajengea uwezo wakulima katika maeneo yao kwa kutoa elimu ya kilimo bora na chenye manufaa ili kupata mazao bora yenye viwango vinavyokubalika ndani na nje ya mipaka ya nchi wanachama.
“Napenda kuzihimiza nchi wanachama kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima wao pamoja na kuwajengea uwezo ili kuwawezesha kuzalisha mazao bora na yenye viwango vinavyokubalika ndani ya jumuiya na nje ili hatimaye wunufaike na soko la ndani na nje ya jumuiya” alisisitiza Dkt. Muthuki kwenye hotuba yake.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Ngazi ya Wataalam, Bw. Julius Mwabu kutoka Jamhuri ya Kenya aliwataka wajumbe wa mkutano huo kujadili na kutoa mapendekezo yenye tija kuhusu Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula kwani ni miongoni mwa sekta muhimu zinazotegemewa na wananchi wote wa nchi wanachama wa Jumuiaya ya Afrika Mashariki.
Aliongeza kuwa, mbali na changamoto ya ugonjwa wa corona uliozikumba nchi mbalimbali duniani zikiwemo zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula na kuwaomba wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ili kuziwezesha nchi wanachama kutotetereka katika kipindi hiki ambacho ugonjwa huo bado haujatokomezwa.


Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Gungu Mibavu na kuhudhuriwa pia na Maafisa Waandamizi kutoka Sekta mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na usalama wa chakula hapa nchini.

Kua wa kwanza kupata taarifa

You may also like...